Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtaka Waziri wa Mifugo, Bashiru Ally, pamoja na watendaji wa sekta hiyo, kuchukua hatua kudhibiti uuzaji wa dawa feki na zisizo na viwango kwa wafugaji nchini.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo leo, Novemba 27, 2026, Ikulu ya Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi wateule, akisisitiza umuhimu wa kusimamia ubora wa dawa zinazouzwa kwa ajili ya mifugo.
“Jambo lingine la kusimamia, wauzaji wa dawa za mifugo wanauza dawa feki, dawa zisizo na viwango kwa wafugaji wetu, hivyo hilo nalo lisimamiwe vizuri,” amesema Rais Samia.
Aidha, amemtaka Waziri Kakuru kuweka utaratibu wa kuyatoa mashamba kwa sekta binafsi ili kushirikiana na Serikali katika ufugaji na uzalishaji wa nyama kwa wingi, akibainisha kuwa kuna soko kubwa la mifugo hai na nyama nje ya nchi ambalo linaweza kutumiwa kukuza uchumi.
Amesema ushirikiano huo utatoa fursa kwa vijana wanaonufaika na Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) kushiriki katika shughuli za ufugaji na uzalishaji kupitia mashamba hayo, hatua itakayoongeza uzalishaji, ajira na tija kwa Taifa.
