Rais Samia Suluhu Hassan, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi unaendelea kuimarika kutokana na historia ndefu ya urafiki na maslahi ya pamoja ya maendeleo.
Akizungumza katika mahojiano aliyofanya na moja ya Kituo cha Televisheni cha Urusi, alipokuwa ziarani nchini humo, Rais Samia amesema Tanzania inafanya kazi na Urusi katika mazingira ya kuelewana na kuheshimiana, jambo linalochangia kuimarika kwa mahusiano ya nchi hizo mbili.
Amesema msingi wa ushirikiano huo unatokana na urafiki wa kihistoria, akitaja mchango wa Urusi katika kuunga mkono harakati za ukombozi wa nchi za Afrika wakati wa mapambano ya kupata uhuru.
Kwa mujibu wa Rais Samia, Urusi imeendelea kuonyesha nia ya kushirikiana na mataifa ya Afrika katika kukuza maendeleo ndani ya mfumo mpya wa uchumi wa dunia unaoendelea kubadilika.
Rais Samia ameeleza Tanzania na Urusi zina dhamira ya pamoja ya kuimarisha ukuaji wa uchumi, kuongeza uwekezaji na kupanua ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wa pande zote, huku zikichangia kufungua fursa mpya za maendeleo kwa bara la Afrika.
