You are currently viewing Rais Samia aikabidhi NBC tuzo ya ufanikishaji wa maadhimisho ya Mei Mosi Njombe

Rais Samia aikabidhi NBC tuzo ya ufanikishaji wa maadhimisho ya Mei Mosi Njombe

Na Mwandishi Wetu, Njombe

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameikabidhi Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) tuzo maalum ya kutambua mchango wake katika kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Lunyanywi, mkoani Njombe.

Tuzo hiyo ilipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw. Theobald Sabi, mbele ya maelfu ya washiriki na viongozi waandamizi wa serikali, akiwemo Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), pamoja na wadau wa sekta binafsi na umma—ikiashiria mshikamano wa kitaifa katika kuthamini mchango wa wafanyakazi kwa maendeleo ya nchi.

Akizungumzia ushiriki wa benki hiyo katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa NBC, Bw. Godwin Semunyu, alisema pamoja na kushiriki maadhimisho hayo, benki hiyo pia ilikuwa miongoni mwa wadhamini wakuu kwa kuchangia shilingi milioni 50 kusaidia maandalizi na uendeshaji wa tukio hilo.

Alisema hatua hiyo inaakisi dhamira thabiti ya NBC ya kuendelea kuthamini na kuwawezesha wafanyakazi, ambao ni mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi wa taifa, kupitia huduma bunifu na jumuishi za kifedha zinazokidhi mahitaji yao.

“Kwetu NBC, Mei Mosi siyo tu siku ya maadhimisho, bali ni fursa ya kuthibitisha upya ahadi yetu ya kuwahudumia wafanyakazi kwa ubunifu, ufanisi na suluhisho bunifu za kifedha zinazokidhi mahitaji yao ya kila siku na ya muda mrefu,” alisema.

Katika kuonesha mshikamano na ari ya kitaifa kwenye maadhimisho hayo yaliyokuwa na kauli mbiu ‘Kazi Zenye Staha ni Nguzo Imara ya Maendeleo Endelevu Katika Utekelezaji Wa Dira ya Taifa 2050’, wafanyakazi wa NBC walishiriki kikamilifu katika maandamano rasmi ya Mei Mosi yaliyopita mbele ya mgeni rasmi, wakionesha umoja wao na wafanyakazi wenzao kutoka sekta mbalimbali nchini.

Aliongeza kuwa NBC imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na wafanyakazi kupitia utoaji wa huduma jumuishi za kifedha zinazolenga kuboresha ustawi wao, ikiwa ni pamoja na akaunti maalum za mishahara, mikopo nafuu ya muda mfupi na mrefu—ikiwemo isiyohitaji dhamana—pamoja na huduma za kidigitali zinazorahisisha upatikanaji wa huduma hizo mahali popote na wakati wowote.

“Huduma zetu za kidigitali kama NBC Kiganjani na NBC Connect zimeleta mageuzi makubwa kwa wateja wetu, hususan wafanyakazi, kwa kuwawezesha kufanya miamala yao kwa urahisi, usalama na ufanisi zaidi,” alisisitiza.

Aidha, Bw. Semunyu aliwapongeza wafanyakazi wa NBC kwa kuendelea kuonesha weledi wa hali ya juu, ubunifu na kujituma katika utoaji wa huduma, jambo ambalo limeendelea kuimarisha imani ya wateja na kuifanya benki hiyo kuwa chaguo linaloaminika kwa taasisi na mashirika mbalimbali nchini.

Katika kuonesha mshikamano na ari ya kitaifa kwenye maadhimisho hayo yaliyokuwa na kauli mbiu ‘Kazi Zenye Staha ni Nguzo Imara ya Maendeleo Endelevu Katika Utekelezaji Wa Dira ya Taifa 2050’, wafanyakazi wa NBC walishiriki kikamilifu katika maandamano rasmi ya Mei Mosi yaliyopita mbele ya mgeni rasmi, wakionesha umoja wao na wafanyakazi wenzao kutoka sekta mbalimbali nchini.