You are currently viewing Rais Samia ameleta ustawi wa wananchi, kukuza uchumi

Rais Samia ameleta ustawi wa wananchi, kukuza uchumi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema falsafa ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeonyesha namna sheria zinavyoweza kuwa chombo cha maendeleo, ustawi wa wananchi na ukuaji wa uchumi badala ya kuwa nyenzo ya adhabu na udhibiti pekee.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha Falsafa ya Sheria ya Rais Samia (Samia Doctrine of Law), Dar es Salaam, amesema kitabu hicho kinachambua uhusiano kati ya sheria, uongozi, taasisi na maendeleo.

Hemed, amesema kitabu hicho kinaakisi kwa kina mageuzi yaliyofanywa chini ya Rais Samia,  katika kujenga maridhiano, kuimarisha taasisi, kuvutia uwekezaji na kuboresha huduma za jamii.

Amesema kitabu kinaonyesha kuwa mapato ya ndani ya Serikali yameongezeka kutoka Sh20.5 trilioni mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh40 trilioni katika bajeti ya 2026/27, hatua inayoongeza uwezo wa nchi kugharamia miradi ya maendeleo kwa kutumia vyanzo vya ndani.

Pia, kinaeleza ongezeko la makusanyo ya VAT kutoka takribani Sh5 trilioni hadi matarajio ya Sh9 trilioni mwaka 2026, sambamba na mageuzi yanayokwenda na ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Kwa mujibu wa Hemed, maboresho ya sheria ya uwekezaji na kuanzishwa kwa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) yameondoa urasimu, kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza mvuto wa Tanzania kwa wawekezaji wa ndani na nje.