Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza kuwa Serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1.
Rais Dkt. Samia amesema kuwa Nyongeza hii itaanza kutumika Mwezi Julai 2025, itaongeza kima cha chini cha mshahara kutoka shilingi 370,000 hadi shilingi 500,000.
Akizungumza Katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Mkoani Singida Dkt. Samia amesema Wafanyakazi wamekuwa na Mchango Mkubwa katika Kuinua Uchumi wa Nchini na ataendelea Kuboresha Maslahi ya Watumishi hao.
“Ninayo furaha kuwatangazia kwamba katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi, mwaka huu serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1. Nyongeza hii itakayoanza kutumika mwezi Julai mwaka huu itaongeza kima cha chini cha mshahara kutoka Sh 370,000 hadi Sh 500,000.

“Ngazi nyingine za mshahara nazo zitapanda kwa kiwango kizuri jinsi bajeti inavyoturuhusu. Lakini nataka niwaambie nyongeza nzuri ipo, amesema na kuongeza;
“Ndugu wafanyakazi, risala yenu imegusia suala la uhuru wa kuunda vyama au kusajili vyama vya wafanyakazi. Kama mnavyofahamu, serikali imeridhia mkataba wa shirika la Kazi duniani namba 87 wa mwaka 1948. Na tunawajibika kuheshimu matakwa ya mkataba huo wa uhuru wa wafanyakazi kujumuika.
“Kwa kulitambua hili, serikali kupitia sheria ya ajira na uhusiano kazini, sura 336, haijaweka masharti yanayozuia usajili wa chama katika maeneo na sekta ambayo tayari kuna vyama vimesajiliwa.”