You are currently viewing Rais Samia atoa bilioni 200/- kuwezesha vijana, wanawake

Rais Samia atoa bilioni 200/- kuwezesha vijana, wanawake

Zile fedha kiasi cha Sh. bilioni 200 kwa ajili ya uwezeshaji biashara za vijana na wanawake sio ahadi tena, tayari Serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeshazitoa na zimepokelewa.

Hatua hiyo, ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Rais Samia wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, alipoahidi ndani ya siku 100 atakapoapishwa kuwa Rais, Serikali yake itatoa Sh. 200 bilioni kuwezesha biashara kwa vijana na wanawake.

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka, hundi ya shilingi bilioni 200 ambazo ni ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya mitaji ya kuwawezesha vijana na wanawake, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, Februari 05, 2026. kulia ni kutoka kwa Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar na kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) William Lukuvi.

Utekelezaji wa ahadi hiyo, unafuatana na ahadi nyingine kadhaa zilizotekelezwa, ikiwemo majaribio ya Bima ya Afya kwa Wote, ajira 7,000 kwa walimu wa sayansi na hesabu na kutozuiwa maiti kwa kushindwa gharama za matibabu katika hospitali za umma.

Makabidhiano ya mfano wa hundi wa kiasi hicho cha fedha yamefanyika jijini Dodoma leo, Alhamisi Februari 5, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar kwenda kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Nchemba amesema kiasi hicho ni nyongeza ya zile fedha ambazo zimekuwa zikitolewa kwa ajili ya makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.

Ametaka masharti ya upatikanaji wa fedha hizo yawekwe wazi ili watu wasiendelee kuogopa, huku akizisisitiza taasisi za fedha kuhakikisha zinalegeza masharti ya uwezeshaji huo.

Leave a Reply