SIKU moja baada ya vituo na mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Saalam (Mwendokasi) kushambuliwa kwa mawe na wananchi, Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa viongozi wanaosimamia mradi huo.
Viongozi waliotumbuliwa ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART). Dkt. Athumani Kihamia pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), Bw. Waziri Kindamba.

Katika taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka, viongozi walioteuliwa kuchukua nafasi hizo ni Bw. Said Habibu Tunda ambaye ameteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi
Yaendayo Haraka (DART). Bw. Tunda anachukua nafasi ya Dkt. Athumani Kihamia ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
“Bw. Pius Andrew Ngingo ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART). Bw. Ng’ingo anachukua nafasi ya Bw. Waziri Kindamba ambaye uteuzi wake umetenguliwa,” imesema taarifa hiyo na kusisitiza uteuzi huo unaanza mara moja.