Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amewaonya wanaoshabikia uvunjifu wa amani nchini, akisema vurugu huishia kupimana nguvu na uwezo wa kujihami, lakini mazungumzo huzaa mshikamano.
Msingi wa onyo hilo la mkuu huyo wa nchi, ni kile kinachofanywa na baadhi ya wanaharakati mtandaoni, kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani nchini.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu Novemba 3, 2025 alipozungumza katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Sita kwa kipindi cha pili, jijini Dodoma.
“Nitumie fursa hii kutoa onyo kama Mama, kutoa onyo kwa wale wote waliochochea uvunjifu wa amani na nawataka watambue kuwa, vurugu na uvunjifu wa amani huishia kupimana nguvu na uwezo wa kujihami, ila mazungumzo huzaa mshikamano, hivyo tuchague lenye manufaa kwetu,” amesema.
Aidha, ameambatanisha ujumbe huo na kile alichoeleza, Tanzania ni muhimu zaidi kuliko matakwa ya mtu binafsi.
Dkt Samia anaapishwa ikiwa ni siku mbili baada ya kuibuka mshindi wa kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Samia alipata asilimia 97.6 ya kura zote, ukiwa ni ushindi mkubwa zaidi kuwahi kupatikana na mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), tangu uhuru wa Tanganyika.
