You are currently viewing Rais Samia kufanya ziara ya kikazi Msumbiji

Rais Samia kufanya ziara ya kikazi Msumbiji

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuondoka nchini leo Juni 24, 2025, kuelekea Maputo, Jamhuri ya Msumbiji kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Katika ziara hiyo, Rais Samia atakuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Msumbiji, kufuatia mwaliko wa Rais wa taifa hilo, Daniel Francisco Chapo. Sherehe hizo zitafanyika katika Uwanja wa Machava, jijini Maputo.

Tanzania inakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa kihistoria katika harakati za ukombozi wa Msumbiji, ambapo iliwahifadhi na kuwasaidia wapigania uhuru wa FRELIMO katika nyakati ngumu za mapambano dhidi ya ukoloni wa Kireno.

Aidha, akiwa nchini humo, Rais Samia atatembelea eneo la kumbukumbu ya mashujaa wa Msumbiji (Mozambican Heroes’ Square) ambako atatoa heshima na kuweka shada la maua kwa ajili ya kuwaenzi waliopoteza maisha katika harakati za ukombozi wa taifa hilo.

Leave a Reply