You are currently viewing Rais Samia kuzindua mpango wa kuboresha afya ya mama na mtoto Afrika

Rais Samia kuzindua mpango wa kuboresha afya ya mama na mtoto Afrika

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasili Addis Ababa, Ethiopia, kwa ziara ya siku mbili, ambapo anatarajiwa kushiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026) na kuzindua Mpango Elekezi wa Kuboresha Afya ya Mama na Mtoto Barani Afrika, Jumatatu, Novemba 23, 2026.

Rais Samia anatarajiwa kuzindua mpango huo akiwa katika nafasi yake ya Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto.

Mpango huo unalenga kuongoza nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kufikia malengo matatu yanayojulikana kama Sifuri Tatu (Three Zeros).

Malengo hayo ni kuhakikisha kila mjamzito anajifungulia katika kituo cha kutolea huduma za afya akisaidiwa na mtaalamu wa afya; kukomesha vifo vya uzazi na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika; pamoja na kuhakikisha kila mtoto anapata chanjo.

Mpango Elekezi huo utatekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030, ukiwa na lengo la kuongeza uwekezaji kutoka kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na wadau wa maendeleo katika kupanua upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wanawake, watoto na vijana barani Afrika.