You are currently viewing Rais Samia: Shughulikieni migogoro ya ardhi msisubiri watu wauane

Rais Samia: Shughulikieni migogoro ya ardhi msisubiri watu wauane

Rais Samia Suluhu Hassan, amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, David Silinde, pamoja na watendaji wa sekta hiyo, kushughulikia kwa wakati migogoro ya ardhi nchini na kuhakikisha wananchi hawafikii hatua ya kuuana.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo, Novemba 27, 2026, Ikulu ya Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi wateule, akisisitiza kuwa watendaji wa ardhi wanapaswa kuwafuata wananchi na kutatua changamoto zao badala ya kusubiri migogoro ikue na kusababisha mauaji.

Kadhalika amesema anaamini kliniki za ardhi zimeanzishwa kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hivyo ni muhimu kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa, hususan katika kutatua migogoro inayohusisha wakulima na wafugaji.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuheshimu mipaka na matumizi ya ardhi iliyopimwa na kukemea tabia za maofisa wasio waaminifu kuuza kiwanja kimoja kwa zaidi ya mtu mmoja.

“Ardhi iliyokwishapimwa iheshimiwe, ilivyopimwa itumiwe vilevile, ikatumiwa kama ilivyokusudiwa,” amesema Rais Samia.

Katika hatua nyingine, amemtaka Kamishna wa Ardhi, Nathaniel Methew Nhonge, kumsaidia Waziri wa Ardhi kufanya maamuzi sahihi kwa kumpatia ushauri wenye tija badala ya kumpotosha au kumwelekeza katika maamuzi yasiyo sahihi.