You are currently viewing Rais Samia wa kwanza kurudisha fomu INEC

Rais Samia wa kwanza kurudisha fomu INEC

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amewatangulia wagombea urais wa vyama vingine kurudisha fomu ya uteuzi katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Ndejengwa jijini Dodoma leo, Jumatano Agosti 27, 2025.

Hatua hiyo, inampa nafasi mkuu huyo wa nchi ya kusubiri uteuzi wa INEC, kisha kuanza mchakamchaka wa kampeni za uchaguzi, zitakazofanyika kwa kipindi cha siku 60.

Rais Dkt Samia ambaye ndiye mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), atazindua rasmi kampeni za uchaguzi huo, kesho Alhamisi Agosti 28, 2025, katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe, Dar es Salaam.

Mgombea huyo wa CCM, amefika katika ofisi za INEC, saa moja na dakika 50 asubuhi, akiwa wa kwanza kabla ya wagombea wengine wa nafasi hiyo, kama alivyofanya wakati wa uchukuaji fomu Agosti 9, 2025.

Rais Dkt Samia ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, alisindikizwa na baadhi ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho, huku akiambatana na mgombea mwenza, Dkt Emmanuel Nchimbi.

Baadhi ya walioambatana naye katika tukio hilo ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Asha Rose Migiro na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Mary Chatanda, sambamba na wajumbe wengine wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).

Leave a Reply