You are currently viewing Rais Samia: Wananchi wote kupata nishati safi ya kupikia ifikapo 2034

Rais Samia: Wananchi wote kupata nishati safi ya kupikia ifikapo 2034

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali inalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda afya za wananchi, kuhifadhi mazingira na kuboresha maisha yao.

Amesema upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini umeongezeka kutoka asilimia 16 mwaka 2022 hadi asilimia 28.6, huku Serikali ikilenga kufikisha kiwango hicho asilimia 35 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2026.

Akizungumza leo Novemba 12, 2026 katika Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika, uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), Antalya, Uturuki, Rais Samia amesema mafanikio hayo yametokana na hatua mbalimbali za Serikali ikiwemo kupanua usambazaji wa umeme vijijini, kupunguza gharama za umeme kwa matumizi ya kupikia, kutoa ruzuku kwa vifaa vya gesi na kuweka vivutio vya kikodi kwa teknolojia za nishati safi.

“Nchini Tanzania, tumeweka lengo la kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa wananchi wote ifikapo mwaka 2034,” amesema Rais Samia.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kupanua upatikanaji wa teknolojia mbalimbali zinazofaa, kuboresha mitandao ya usambazaji na kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi, hususan katika maeneo ya vijijini na yale ambayo bado hayajafikiwa vya kutosha na huduma hizo.

Kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha, hadi Machi 2026, Serikali ilikuwa imewezesha usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia zaidi ya 346,000 kwa bei ya ruzuku, majiko ya umeme ya induction zaidi ya 49,000 na majiko mengine ya umeme 7,000. #TanzaniaCOP31