Rais wa shirika la ndege la Emirates, Sir Tim Clark, amesema shirika hilo halitapokea kundi la kwanza la ndege 10 za Boeing 777X, akieleza kuwa ucheleweshaji mrefu umefanya ndege hizo zisiwe na manufaa.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Anga ya Farnborough, Sir Tim alisema kundi hilo la kwanza litahitaji marekebisho mengi kiasi kwamba halitakuwa tena la kufaa kwa matumizi.
“Hatutapokea kundi hilo na hivyo ndivyo ilivyo,” alisema.
“Kwa mtazamo wetu, wao wajue cha kufanya nazo.”
Pia aliongeza kwa mzaha kuwa, ndege hizo “zitakuwa bora zikageuzwa kuwa makopo ya maharagwe ya kuokwa”.
Emirates ina jumla ya oda ya ndege 270 za 777X kutoka Boeing, kila moja ikiwa na thamani ya takriban dola milioni 440 au pauni milioni 330, huku ndege ya kwanza ikiwa imetengenezwa mwaka 2019.
Hata hivyo, ucheleweshaji wa mara kwa mara kutokana na mabadiliko ya muundo umesababisha Emirates kusubiri ndege hizo kwa miaka saba bila kuzipokea. Boeing bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu uamuzi huo wa Emirates.
