Rais wa Kenya, William Ruto ameomba radhi mataifa jirani ya Tanzania na Uganda katika hatua ambayo inaonekana kuwa ni juhudi za kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo ya Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa dhifa ya kifungua kinywa cha Kitaifa katika jijini Nairobi, Rais Ruto alitoa wito wa kurekebishwa kwa uhusiano, akibainisha kuwa Kenya iko kwenye njia ya kuinuka na kujenga upya.
“Jirani zetu wa Tanzania kama tumewakosea kwa namna yoyote tunaomba radhi, wenzetu wa Uganda ikiwa kuna jambo ambalo Wakenya wamefanya ambayo sio sahihi tunataka kuomba radhi,” alisema Rais Ruto.
Kauli ya Ruto inakuja wakati ambapo mvutano umeibuka kufuatia hatua ya Tanzania kuwatimua wanaharakati wa Kenya waliokuwa wamesafari hadi nchini humo kushuhudia kusikilizwa kwa kesi kiongozi wa upinzani Tundu Lissu.
Tukio hilo limesababisha majibizano makali kati ya nchi hizo mbili za Afrika Mashariki huku watumiaji wa mtandao wakiwa katika mzozo wa muda mrefu kuhusu siasa za kikanda na uanaharakati.