Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, amezindua mpango mpya wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) wa utoaji wa vyeti vya kuzaliwa ndani ya saa 48 za kazi, kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ikiwa ni hatua ya kuharakisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi.
Uzinduzi wa mpango huo umefanyika jijini Dar es Salaam ambapo Dkt. Homera ameitaka RITA kusimamia na kutekeleza mpango huo kwa weledi wa hali ya juu, akibainisha kuwa uzoefu wa RITA unatosha kufanikisha azma hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Homera alisema mpango huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyesisitiza kuwa vyeti vya kuzaliwa vipatikane ndani ya saa 48 za kazi.

“Mfumo huu tuliouzindua ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, kuhakikisha vyeti vya kuzaliwa vinapatikana kwa wakati, ili wananchi wapate huduma nyingine muhimu zinazotegemea cheti hicho,” alisema Dkt. Homera.
Alifafanua kuwa zoezi la kupata cheti cha kuzaliwa litakuwa rahisi endapo waombaji watakuwa na viambatanisho muhimu, ikiwemo barua ya Serikali ya Mtaa, taarifa za hospitali pamoja na vielelezo kutoka taasisi za dini kama misikiti na makanisa.
Aidha, Waziri Homera aliipongeza RITA kwa mafanikio makubwa waliyoyapata, akisema kuwa hadi kufikia Novemba 25 mwaka huu, wamefanikiwa kutoa vyeti vya kuzaliwa milioni 11.5.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za RITA, jumla ya Watanzania milioni 20 wamefanikiwa kusajiliwa hadi Novemba 2025, ikilinganishwa na Watanzania 205,000 pekee waliokuwa wamesajiliwa mwaka 2004.
Katika hatua nyingine, aliitaka RITA kuendelea kusimamia kwa ufanisi taasisi zote zilizo chini yake pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya uandishi na usimamizi wa mirathi, ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima katika jamii.
Kwa upande wake, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Bw. Frank Kanyusi alisema mahitaji ya vyeti vya kuzaliwa ni makubwa, na kwamba mpango huo mpya utasaidia kupunguza msongamano wa wananchi wanaosubiri huduma katika taasisi mbalimbali za umma.

“RITA ndiyo taasisi ya kwanza kutoa utambulisho rasmi wa Mtanzania pale tu anapozaliwa na cheti hiyo ni muhimu sana katika upatikanaji wa huduma nyingine kutoka mbalimbali hapa nchini ikiwemo upatikakanaji wa hati ya kusafiria na mengineyo,” amesema.
Akielezea mafanikio mengine ya taasisi hiyo, Bw. Kanyusi amesema kuwa hadi Novemba 25 mwaka huu, RITA imefanikiwa kufanya usajili wa vyeti vya ndoa zaidi ya milioni moja, vyeti vya vifo zaidi ya elfu 12, pamoja na maboresho mbalimbali ya kiutawala na kidijitali.
Mmoja wa wananchi aliyenufaika na mpango huo, Bi. Fatuma Saidi, alisema alipata cheti cha kuzaliwa cha mtoto wake ndani ya saa 48 za kazi, jambo ambalo halikulitarajia.
“Nilitegemea kupata cheti ndani ya wiki mbili au tatu, lakini nilishangaa kuambiwa ndani ya saa 48 kuwa cheti changu kiko tayari,” alisema Bi. Fatuma.
