Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imepokea madai 248 kutoka kwa wadau na taasisi mbalimbali kwa iliyokuwa kampuni ya kukopesha fedha ya Pride Tanzania ili waweze kuchakata na kubaini uhalisia wa madai hayo na kuyatolea ufafanuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema wiki hii jijini Dar es Salaam, Kabidhi Wasihi Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bw. Frank Kanyusi amesema waliteuliwa na Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Arusha kusimamia mchakato wa ufilisi wa taasisi hiyo ya kifedha nchini, na miongoni mwa majukumu yao ni kupata taarifa sahihi za kampuni hiyo kwa kukusanya taarifa za watu wanaodaiwa na wanaoidai kampuni hiyo.
“Mnamo Novemba 7, 2025 tulipokea uteuzi kutoka mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha kupitia maombi namba 2272 ya mwaka 2025 kuwa mfilisi wa Pride” alisema Bw. Kanyusi.
Alisema baada ya uteuzi huo wa Mahakama kuu, Januari 26, 2026 Wakala ulitoa notisi kwa umma ya kuwataka wadai wote kuwasilisha taarifa na uthibitisho wa madai yao kwa Wakala ndani ya siku 14 tangu tarehe ya kutolewa kwa notisi hiyo hadi Februari 8, 2026.
“Kwa majuma hayo mawili tumepokea malalamiko 248 wa madai kwa kampuni hii ya Pride kutoka kwenye makundi mbalimbali ya watu na taasisi nyingine za kifedha kama vile wafanyakazi, mabenki na vikundi vinginevyo vya fedha” alibainisha Bw. Kanyusi.
Pamoja na hayo alibainisha kuwa madai ya wafanyakazi yalikuwa 111 ambayo ni pamoja na malimbikizo ya mishahara, madai ya fedha za usafiri na mengine, lakini pia taasisi nyingine tisa za zabuni zilikuwa zinadai fedha za kusambaza vifaa mbalimbali kwenye taasisi hiyo kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.
“Pamoja na hayo tumepokea madai 70, ambayo hayajawekwa wazi kuwa wanadai nini katika kampuni hiyo, kwani utaratibu wetu uliwataka wanaodai wote wasema madai yao ni nini na waambatanishe na ushahidi wa madai hayo” alieleza Bw. Kanyusi.
Bw. Kanyusi alisema ijapokuwa kuna wengine hawajawasilisha taarifa za kudaiwa na kampuni hiyo, wao wataendelea na utafiti wao ili waweze kubaini wadaiwa wote wa kampuni hiyo.
Kampuni ya mikopo ya Pride ilisajiliwa rasmi Mei 5, 1993 kwa lengo la kutoa mikopo isiyo na dhamana kwa vikundi vya wajasiriamali wadogo wadogo wa vijijini ili kuwakwamua kiuchumi.
