You are currently viewing Rodri ashinda Ballon d’Or

Rodri ashinda Ballon d’Or

Kiungo wa kati wa Uhispania na Manchester City, Rodrigo Hernández Cascante ‘Rodri’ ameshinda tuzo ya Ballon d’Or ya mchezaji bora wa dunia kwa mwaka 2024, akiwashinda Mbrazil Vinicius Jr na Muingereza Jude Bellingham, wote wa Real Madrid, kwa tuzo hiyo ya kifahari.

Rodri alishinda taji la Ligi ya Premier ya England na la Euro 2024. Uamuzi wa kumtuza kiungo huyo mkabaji ilijiri kwa mshangao, kwa vile mshindi wa taji la La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya Vinicius Junior wa Real Madrid alionekana kupigiwa upatu na wengi.

Saa chache kabla ya hafla hiyo ya jana Jumatatu usiku mjini Paris, klabu hiyo ya Uhispania ilitangaza kuwa ujumbe wake hautahudhuria sherehe hiyo kwa sababu ya kile ilichokichukulia kuwa ni kutotendewa haki Vinicius.

Rodri, 28, alichangia pakubwa wakati City ikiizuia Arsenal kushinda Ligi kuu ya England msimu uliopita na alitajwa kuwa mchezaji bora wa mashindano ya Euro 2024 wakati Uhispania iliibuka mshindi nchini Ujerumani.

Rodri alitumia lugha ya kidiplomasia wakati akizungumzia suala la Real kutoonekana kwenye hafla hiyo. “Wana uamuzi wao, hawakutaka kuwa hapa kwa sababu zao,” alisema. “Ninaangazia tu klabu yangu na wachezaji wenzangu.”

Hata hivyo, Vinicius amesema ataendelea kupiga vita ubaguzi wa rangi hata kama harakati zake ndizo zilifanya asishinde Ballon d’Or.

Hayo ni kwa mujibu wa vyanzo vilivyo karibu na mchezaji huyo.

Baada ya kuorodheshwa wa pili katika tuzo hiyo, aliandika kwenye mitandao ya kijamii. “Nitafanya mara kumi zaidi kama lazima nifanye hivyo. Hawako tayari,” aliandika Vinicius, (24) kwenye X.

Usimamizi wake ulieleza kuwa alimaanisha ataendeleza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na anaamini ndicho kilifanya asishinde tuzo hiyo, akisema kuwa “ulimwengu wa kandanda hauko tayari kumkubali mchezaji anayepigana dhidi ya mfumo.”

Vinicius alifunga magoli 24 na kutoa asisti 11 katika mechi 39 kwenye mashindano yote wakati akiiongoza Madrid kubeba mataji matatu msimu uliopita.

“Kama vigezo vya tuzo havimpi ushindi Vinicius, basi vigezo hivyo hivyo vinapaswa kumpa Carvajal ushindi,” imesema Real Madrid.

“Kwa sababu haijawa hivyo, ni wazi Ballon d’Or-UEFA hawaheshimu Real Madrid. Na Real Madrid haiendi mahali ambako haiheshimiwi.”

Ujumbe wa Madrid waliokuwa kwenye orodha ulijumuisha Kylian Mbappe, Antonio Rudiger, Fede Valverde na Jude Bellingham.

Tuzo hizo zinatokana na upigaji kura wa jopo la waandishi wa habari za michezo kutoka nchi 100 za juu katika orodha ya viwango vya FIFA. Real Madrid ilishinda tuzo ya timu bora wakati Carlo Ancelotti akishinda Kocha bora.

Leave a Reply