Baada ya kuiongoza Manchester United kwa ushindi wa mechi nne mfululizo, hatimaye kocha Ruud Van Nistelrooy amebwaga mikoba ya ukocha klabuni hapo na kumpisha Ruben Amorim kuendelea kuongoza klabu hiyo.
Mkataba baina ya klabu ya Manchester United na Amorim unaanza rasmi leo Jumatatu tarehe 11 Novemba na unatarajiwa kukamilika Juni mwaka wa 2027.
Manchester United ililazimika kukatisha mkataba wao na kocha aliyefutwa Erik Ten Hag baada ya kupoteza mechi ya ligi kuu nchini Uingereza dhidi ya Westham kwa kupigwa mabao mawili kwa moja mnamo Oktoba 27.
Ruud van Nestelrooy, alitwikwa majukumu ya kuongoza Man United baada ya kutimuliwa kwa Erik Ten Hag kutokana na matokeo mabovu akichukua nafasi ya kocha kaimu hadi Jumatatu 11 ambapo kocha mpya wa Man United alitakiwa kuingia kambini Old Trafford.
Baada ya kuchukua uongozi wa Man United, katika mechi nne ambazo ameongoza miamba hao wa soka kutoka jiji la Manchester, Ruud hajapoteza mechi hata moja. Kocha huyo ameshinda mechi tatu na kutoka sare mechi moja dhidi ya Chelsea.
Man United ililazimika pia kulipa takribani pauni milioni 8 ili kupata huduma za Ruben Amorim kwani alikuwa na mkataba tayari na timu ya Spoting CP.
Anapoingia Man United, kocha Amorim ana kibarua cha kuikwamua Man United ambayo kufikia sasa inashikilia nafasi ya 13 kwa alama 15 baada ya mechi 11 za msimu 2024/2025.
Aidha, Man United katika ujumbe wa kumuaga Ruud van Nestelrooy kwenye mtandao wa X imesema, “umetufanya tujivunie, Ruud.”