Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), imempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa na kuapishwa kuiongoza Tanzania kwa kipindi cha pili, katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Sambamba na pongezi hizo, jumuiya hiyo imeeleza kusikitishwa na imetoa salamu za rambirambi kutokana na vifo na uharibifu wa mali za watu binafsi na miundombinu ya umma, uliofanywa wakati wa vurugu za siku ya uchaguzi.
Pongezi hizo zimetolewa Alhamisi Novemba 7, 2025 katika mkutano mkuu maalumu wa wakuu wa nchi wanachama wa SADC kwa njia ya mtandao, uliohudhuriwa na viongozi wa mataifa 15, huku Tanzania ikiwakilishwa na Makamu wa Rais, Dkt Emmanuel Nchimbi.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja (Communique), SADC inatuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao wakati wa maandamano yaliyotokea Madagascar na vurugu za hivi karibuni nchini Tanzania.
“Mkutano ulielezea masikitiko makubwa kwamba matukio haya yalisababisha sio tu upotevu wa maisha, bali pia uharibifu wa mali za umma na miundombinu muhimu katika mataifa yote mawili,” imeeleza taarifa hiyo ya wakuu wa nchi.
Pia, mkutano ulitambua uamuzi wa Madagascar wa kuachia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Sadc kufuatia hali ya kisiasa ya hivi karibuni ambayo imeathiri uwezo wake wa kutekeleza majukumu katika nafasi hiyo.
Mkutano huo ulitambua kwamba, kwa mujibu wa Kifungu cha 9A(2)(b) na 10(4) cha Mkataba wa SADC, Mwenyekiti anayeingia (Naibu Mwenyekiti) atachukua uongozi wa muda endapo Mwenyekiti aliyepo hatoweza kutekeleza majukumu yake.
“Kwa muktadha huu, Jamhuri ya Afrika Kusini iliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa muda wa SADC hadi Agosti 2026. Sekretarieti ya SADC itashirikiana na nchi wanachama, kwa kuzingatia kanuni ya mzunguko wa uongozi ili kumtambua Mwenyekiti anayeingia (Naibu Mwenyekiti) mpya kufikia Novemba 30, 2025,” inaeleza taarifa hiyo.
