Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan ameahidi kushughulikia suala la upatikanaji wa Katiba Mpya, akisema ni takwa la makundi mbalimbali ya Watanzania.
Dkt Samia amesema CCM inatambua umuhimu wa kuimarisha mshikamano wa Watanzania kwa kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa mchakato Katiba Mpya, kama ilivyoanishwa katika Ilani ya Uchaguzi 2025-30 ya chama hicho.

“Kwa nyakati tofauti tulijaribu suala hili, hasa Serikali ya awamu ya nne lakini mchakato haukukamilika. Awamu ya sita tunakwenda kuuendeleza mchakato huo,” amesema Dkt Samia.
Mgombea huyo, ameeleza hayo leo Ijumaa Oktoba 10,2025 katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika uwanja wa Mwenge, wilayani Butiama mkoani Mara, kwenye mwendelezo wa kusaka kura zitakazomwakikishia ushindi katika uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Katika mkutano huo, Dkt Samia amewahakikishia wananchi wa Butiama kwamba kama ambavyo waasisi na wazee wa Taifa hili kuhusu kulinda nafasi ya Chama cha Mapinduzi, naye ataendeleza hilo katika kusimamia masuala yote kwa masilahi mapana ya Watanzania.
“Baba wa Taifa (Julius Kambarage Nyerere), alisema bila CCM Madhubuti nchi yetu itayumba, hatukubali nchi yetu iyumbe kwa kisingizio chochote kile,” Dkt Samia
Dkt Samia ambaye kabla ya kufika katika mkutano huo, alizuru kaburi la Baba Taifa, Mwalimu Nyerere eneo la Mwitongo, ambapo amewaambia WanaButiama kuwa Serikali yake itaendelea kudumisha tunu za amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, sambamba na Muungano.
Dkt Samia amewaahidi wananchi wa Butiama kwamba Serikali yake itahakikisha inaboresha huduma za kijamii ikiwemo umeme, elimu na maji awamu ya pili ya uongozi wake ataendeleza kuboresha huduma hizo kwa kasi ileile.
“Sehemu ambayo maji hayafiki tutahakikisha yanafika, pale ambalo umeme haujafika, tutahakikisha unafika.Pale ambapo hakuna shule, nyumba za walimu hakuna, tunakwenda kutekekeleza, pale ambapo huduma za afya ziko mbali, tutazisogeza kwa ukaribu, tutaendelea na kasi ileleile,” amesema Dkt Samia.
