Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan, ametangaza mpango wa kuzinyanga’nya mashamba ya Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania (METL) na Watco ili kuyagawa kwa vyama vya ushirika.
Uamuzi huo, umefikiwa baada ya kampuni hizo, kushindwa kuyaendeleza mashamba hayo, huku wakulima hasa wa chai wilayani Rungwe wakilalamikia kukosa maeneo ya kilimo.

Dkt Samia ametangaza msimamo huo leo Ijumaa, Septemba 5, 2025 wakati akiwahutubia wananchi wa Mji wa Tukuyu wilayani Rungwe katika mkutano wa hadhara ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za kusaka kura za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Kabla ya kutangaza ahadi, Dkt Samia amesema awali kampuni hizo zilikabidhiwa mashamba kwa kuamini sekta binafsi itafanya kazi na Serikali ili kuleta na kukuza maendeleo ya wananchi.
Amefananua kuwa Serikali iliweka mazingira mazuri ya uwekezaji, sheria, sera na mambo mengine ya kufanya kazi ndio maana miundombinu ya umeme, maji na barabara inaboreshwa ili kurahisisha shughuli hiyo.
“Tulikubaliana na wenzetu hawa (METL na Watco) kuwapa mashamba na kuweka viwanda ili chai iongezwe thamani kabla ya kusafirishwa,kinachoonekana hii kazi imewashinda.
“Serikali imeunda timu inayofanya tathmini ya mashamba na viwanda, lengo kuyachukua mashamba na viwanda na kuyamikilikisha kwa vyama vya ushirika chini ya uongozi wa Serikali,” amesema Dkt Samia.
Pamoja na kampuni hizo kunyang’anywa mashamba hayo, Dkt Samia amewahakikishia wakulima na wafanyakazi wa viwanda hivyo vitakavyorejeshwa serikalini kuwa, madeni wanayoyadai kwa wamiliki wa viwanda hivyo yatalipwa.
“Tunajua watu hawa wana madeni kwa wafanyakazi kazi wao wa viwanda na wakulima, nataka niwaambie tumewaekeleza waanze kulipa madeni ya watu.
“Tumewajengea mazuri mazuri na benki ili kupata mikopo kulipa madeni, tunakwenda kusimamia lazima madei yalipwe. Madeni lazima yalipwe kabla ya Serikali haiachukua mashamba na kuyamilikisha kwa vyama vya ushirika, nawaahidi si muda mrefu yatakuja kulipwa,”amesisitiza Dkt Samia katika hotuba yake.
