Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema katika miaka mitano ijayo, Serikali yake itaangalia uwezekano wa kuipanua Barabara ya Kilwa kutoka Kongowe hadi Mkuranga.
Uamuzi wake huo, unatokana na kile alichofafanua, anatambua barabara hiyo inakabiliwa na msongamano wa magari na kuathiri shughuli za usafiri na usafirishaji wa abiria na bidhaa, hivyo kudumaza uchumi wa wananchi.

Dkt Samia ametoa ahadi hiyo leo, Jumatatu Oktoba 20, 2025 alipozungumza na wananchi wa Mkuranga, katika mkutano wake wa kampeni za urais, uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.
Amesema anatambua kuwepo kwa msongamano wa magari katika Barabara ya Kilwa hasa kipande cha kutoka Kongowe, hali inayochangia ucheleweshaji wa shughuli za usafiri na usafirishaji wa bidhaa na abiria na hivyo kuathiri uchumi.
“Tunaangalia uwezekano wa kufanya upanuzi wa barabara hii ya Kilwa kutoka kongowe hadi Mkuranga. Kwa sababu mna jembe mliloniletea (Abdallah Ulega) na nimelikabidhi Wizara ya Ujenzi, naona yeye atapekuapekua huko aone nini kinaweza kufanyika,” amesema.
Sambamba na hilo, ameahidi ujenzi wa Barabara ya Mkuranga Mjini hadi Kisiju yenye urefu wa kilomita 40, akilenga kuifungua Bandari ya Kisiju ianze kufanya kazi.
Dkt Samia pia, ameahidi ujenzi wa Stendi ya Mabasi kubwa kwa ajili ya wasafiri kwenda mikoa ya kusini, kwani tayari eneo limeshatengwa na wananchi.
