You are currently viewing Samia awataka waganga kutafuna mafungu ya wagombea badala ya ramli chonganishi

Samia awataka waganga kutafuna mafungu ya wagombea badala ya ramli chonganishi

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka waganga wa tiba asili kuacha kupiga ramli chonganishi ili kuifanya Tanzania ivuke salama kwenye uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 2025.

Amewataka waganga hao kula pesa za wagombea wanaoonekana kuangukia pua katika uchaguzi huo badala ya kuwaaminisha kuwa ni ndugu au wagombea wenzao ndio watawaangusha.

Aidha, Watanzania kushiriki kikamilifu kulinda maadili kwa ajili ya ustawi wa jamii kwa kuwajukumu hilo ni la Watanzania.

Rais Dkt. Samia ameyasema hayo jana Jumamosi wakati wa ufunguzi rasmi wa Tamasha la Utamaduni la Bulabo lililofanyika katika viwanja vya Bujora-Kisesa, Wilayani Magu.

Aidha, Rais Dkt. Samia amesemna Serikali inatambua na kuthamini juhudi kubwa zinazofanywa na wadau wa utamaduni pamoja na viongozi wa kimila katika kuhakikisha utamaduni wa Tanzania unaenziwa na kurithishwa kizazi hadi kizazi.

Vilevile, Rais Dkt. Samia ameeleza Serikali inatambua umuhimu wa matamasha ya utamaduni na itaendelea kuyatumia katika kudumisha na kuendeleza utamaduni, mila na desturi za Watanzania.

Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa utamaduni ndio msingi mkuu wa utambulisho na mshikamano wa Taifa hususan katika kipindi hiki cha mabadiliko ya dunia katika nyanja za kiteknolojia, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Halikadhalika, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha Tamasha la Bulabo linatangazwa na kutambulilka kimataifa kutokana na upekee wake katika kuhifadhi utamaduni.

Aidha, Rais Dkt. Samia amewapongeza waandaaji wa Tamasha la Utamaduni la Bulabo la mwaka huu kwa maandalizi mazuri yaliyovutia wageni kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo Oman na Jamhuri ya Afrika Kusini, na hivyo kulifanya tamasha hili kuanza kusikika kimataifa.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amepongeza jitihada za Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendesha mafunzo sambamba na Tamasha hilo kuhusu umuhimu wa kulinda na kudumisha maadili, mila na desturi za Kitanzania, na kueleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kurithisha utambulisho na tamaduni za Taifa kwa vizazi vijavyo.

Mapema kabla ya kufungua Tamasha, Rais Dkt. Samia alitembelea Kituo cha Utamaduni cha Bujora na Makumbusho ya Kabila la Wasukuma na kuzungumza na Machifu na Watemi wa kabila hilo.

Rais Dkt. Samia amnewaomba viongozi wa kimila, Machifu na Watemi kuendelea kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano wa Taifa.

Rais Dkt. Samia amehitimisha rasmi ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza na kuwashukuru wananchi wote wa Mkoa huo kwa ushirikiano mkubwa na ukarimu waliomuonesha wakati wote wa ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Leave a Reply