Rais Samia Suluhu Hassan amesema amani na utulivu ni mtaji mkubwa kuliko fedha katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, akisisitiza kuwa bila mazingira ya amani malengo hayawezi kutekelezwa.
Akizungumza leo Agosti 3, 2026 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Nyenzo za Utekelezaji wa Dira 2050 iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema hata kama nchi itakuwa na rasilimali nyingi za kifedha, bila amani na utulivu haitawezekana kufanikisha dira hiyo.
“Unaweza kuwa na trilioni za fedha lakini bila amani na utulivu hii dira haitotekelezeka na hatutaweza kufanya chochote,” amesema Rais Samia.
Amewataka Watanzania wote pamoja na sekta za umma na binafsi kuendelea kuilinda amani ya nchi, akieleza kuwa mazingira tulivu humwezesha mfanyabiashara kufanya kazi bila hofu, jambo linalochochea uwekezaji, biashara na ukuaji wa uchumi.
“Katika safari yetu ya Dira 2050 ni wajibu wetu kulinda amani na utulivu. Tukilinda amani na utulivu tutakuwa tumelinda uwekezaji, ajira, biashara na kasi ya ukuaji wa uchumi,” amesema.
