MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasihi wananchi waendelee kumwamini kwa kumpa kura nyingi za ndiyo kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika awamu yake ya kwanza ya uongozi.
Akizungumza katika mikutano tofauti ya hadhara aliyoifanya mkoani Tabora anakoendelea na ziara yake yake ya kampeni, Rais alitaja utekelezaji wa miradi tofauti ya afya, elimu na maji aliyosema imebadili maisha ya Watanzania
“Mkakipigie kura Chama Cha Mapinduzi kwa sababu tunajiamini tumetekeleza na tunajiamini tutatekeleza, kwa hiyo tupeni ridhaa yenu tukawatumikie,” amesema Dkt Samia.
Mgombea huyo amesema siri ya mafanikio hayo ni hatua ya serikali yake kudhibiti mianya ya rushwa, kulikosababisha fedha zitumike kama ilivyopaswa, huku Tanzania ikipanda hadhi katika udhibiti wa ufisadi.
Ameeleza ni matarajio yake kuwaona wananchi kwa wingi kwenye boksi la kura wakienda kumpigia kura.
Katika hatua nyingine, amesema kila mradi uliotekelezwa chini ya Serikali yake ni matokeo ya mikakati imara ya kudhibiti rushwa na ubadhilifu.
“Miradi imewezekana kujengwa Tanzania nzima na kila unaposimama hadithi ni hii hii, umeleta maji, umeleta umeme, umeleta kilimo, umeleta afya kutoka na Serikali kusimamia vema matumizi ya fedha kwa kuwafanya watumishi waepuke rushwa.
“Hizi fedha tungeacha mianya ya rushwa, tungeacha kusimamia vizuri fedha hizi, miradi tunayozungumza leo isingekuwepo. Kwa hiyo Tanzania kwa upande mwingine tumefanya kazi kubwa, kupunguza sisemi hakuna, lakini kama ipo kwa kiwango kidogo sana,” amesema.
Amesema hata tafiti za kimataifa zinaonyesha kila mwaka Tanzania inapanda juu katika viwango vya kupunguza rushwa kwenye shughuli zake.
Kwa mujibu wa Dkt Samia, kwa hatua hiyo watumishi wa sekta ya umma, binafsi na wengine wanastahili kupongezwa.

Akizungumzia Nzega, amesema tayari ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) mkoani Tabora, umeshafikia asilimia 60 na kwamba atahakikisha unakamilika ili vijana wasome.
Ameeleza ujenzi huo, unalenga kuwapa ujuzi vijana wa Nzega na kwamba watafundishwa kilimo na ufugaji kwa kuwa ndizo shughuli kuu katika eneo hilo.
Amesema wanawapa ujuzi huo, ili vijana hao wajiajiri au kuajiriwa kwenye kongani za viwanda zitakazojengwa na Serikali chini yake, pale atakapochaguliwa kuingoza tena Tanzania.
Mengine yaliyofanywa naye katika mkoa huo, amesema ni kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo katika machimbo ya Lusu mkoani humo, ili waendelee na uchimbaji madini.
Amesema ataendelea kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa mipango mbalimbali ili waendelee kuongeza mchango katika mapato Serikali.
Ameahidi kujenga machinjio nne na majosho sita kwa ajili ya mifugo wilayani Nzega, huku ruzuku ya chanjo kwa mifugo ikiendelea kutolewa katika Serikali yake mpya.
Ameahidi kuendelea kuimarisha upatikanaji wa maji kupitia awamu ya pili ya mradi wa Ziwa Victoria utakaowanufaisha wananchi 85,607 mkoani Tabora.
Lingine aliloahidi, amesema ni ujenzi wa barabara ya Nzega-Itogo-Kagongwa yenye urefu wa kilomita 65. #Tunatikisamia