Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwani matokeo ya ruzuku hizo yamekuwa ni makubwa hususani kwa Mkoa wa Mbeya ambako wanazalisha zaidi mazao ya pareto, mahindi, mpunga na maparachichi na asilimia 85 ya wananchi wake ni wakulima.
Amewahakikishia kwamba uwezo wa Serikali kutoa ruzuku bado upo, hivyo amewataka wajisajili na kutunza namba za siri huku akionya kwamba mbolea za ruzuku siyo kwa ajili ya kuuzwa.

“Nakumbuka nilipokuja hapa mlinieleza kwamba hitaji lenu kubwa ni mbolea. Nililifanyia kazi, mbolea imegawiwa na wakulima wamenufaika. Lengo letu tuzalishe, tujilishe na ziada tuuze kama mazao ya biashara. Tanzania tuna ziada ya chakula, niwashukuru sana wakulima.
“Niwaombe sana wakulima, mkajisajili kupata ruzuku ya pembejeo kwani uwezo wetu wakutoa ruzuku upo. Mbolea tunazotoa kwa ruzuku siyo kwa ajili ya kuuzwa, msishirikiane na waovu kuuza vitu vinavyotolewa kwa ruzuku,” amesema.