Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Dkt Samia Suluhu Hassan, amewaambia wananchi wa Tabora kuwa atajenga barabara ya mzunguko yenye urefu wa kilomita 82 ili kupunguza msongamano mkoani humo.
Ameeleza hayo, leo Ijumaa Septemba 12,2025 wakati akihitimisha kampeni zake za mkoa wa Tabora kabla ya kuelekea mkoani Kigoma kuendelea kusaka kura kupitia mikutano ya hadhara iliyoandaliwa na CCM.

Huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi wa Tabora, Dkt Samia,amesema awamu ya pili, endapo atapata ridhaa Serikali atakayoingoza itajenga barabara ya mzunguko ili kupunguza msongamano ndani ya manispaa ya Tabora.
“Ninayo furaha kuwaeleza kuwa tunakuja na ujenzi wa barabara mpya ya mzunguko ya Tabora Mji. Tumeshafanya tathimini ya barabara hii itakayokuwa na urefu wa kilomita 82”
“Hii itahakikisha magari yote yasiyokuwa na ulazima wa kupita ndani ya mji wa Tabora, yanapita barabara ya nje kwenda yanakoelekea.Tunataka Tabora yenye historia kubwa, iwe na hadhi kubwa pia,”amesema Dkt Samia.
Mbali na hilo, Dkt Samia amesema awamu ijayo watajenga madaraja 133 katika barabara zilizowekwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2025/30 zikiwemo zilizoombwa na mkoa wa Tabora.
“Tunakwenda kuweka taa za barabarani 2,300 kwa hiyo Tabora na wilaya zake zitapata fursa ya kufanya biashara kwa saa 24.Tunataka vijana wetu wapate fursa ya kufanya biashara kwa saa 24,” amesema Dkt Samia.