Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake ipo katika majadiliano na Taifa la India na wazalishaji wengine wa mbaazi, kuhakikisha bei ya zao hilo haishuki kupitiliza.
Dkt Samia ameyasema hayo leo, Ijumaa Oktoba 3, 2025 alipozungumza katika mkutano wa kampeni za urais, uliofanyika katika Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, ambao ni miongoni mwa mikoa inayozalisha mbaazi.
Amesema mwaka huu zao la mbaazi limezalishwa zaidi duniani, hatua iliyosababisha kuporomoka kwa bei yake. Licha ya hatua hiyo, Serikali inafanya juhudi kuhakikisha wakulima wanauza kwa faida.
Amefafanua tayari kuna majadiliano na India kuona namna itakavyowezekana kuhakikisha angalau bei iuzwe angalau si chini ya asilimia 70 ya ile ya mwaka jana.
“Najua wanaotaka kushusha bei wana lawama nyingi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, lakini mfumo huu huu ndio unaofanya kazi, bei zikipanda pia,” amesema.
Amewasihi wakulima wa zao hilo wasivunjike moyo kwa kile alichoeleza, Serikali iko nao.
