You are currently viewing Samia: Tunakwenda kujenga Bandari Bagamoyo

Samia: Tunakwenda kujenga Bandari Bagamoyo

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM),Dkt Samia Suluhu Hassan amesema mradi wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo unakwenda kujengwa eneo la Mbegani mkoani Pwani.

Amesema hatua hiyo, imetokana na upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi huo, unaojumuisha eneo huru ya biashara kukamilika.

Kwa mujibu wa Dkt Samia, ujenzi huo utatekelezwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Reli Tanzania (TRC) na sekta binafsi.

Dkt Samia ameeleza hayo leo Jumapili Septemba 28,2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni wilayani Kibaha mkoani Pwania katika mwendelezo wa kusaka kura za urais.

Amefafanua kuwa Bandari ya Bagamoyo itaunganishwa na reli ya SGR kwa kiliomita 100 kutoka bandari kavu ya Kwala, pia itakuwa na gati za kisasa, ndefu zenye uwezo wa kupokea meli kubwa zaidi za bandari ya Dar es Salaam

“Bandari Bagamoyo itajengwa sambamba na eneo la kiuchumi hekta 9,800 litakalochochea uzalishaji na kuvutia uwekezaji wa viwanda. Ndugu zangu hii ni miradi ya kimapinduzi kufanyika mkoa wa Pwani kuwa kitovu cha usafirishaji nchini,”

“Itaongeza fursa na biashara kwa wananchi na Tanzania kwa ujumla.Ahadi yetu ni kuisimamia na kuiendeleza miradi hii muhimu kwa maendeleo yetu na nchi kwa ujumla,” amesema Dkt Samia.

Mbali na hilo, Dkt Samia amesema idadi ya viwanda vinavyojengwa mkoa wa Pwani imeongezeka kutoka 1,387 mwaka 2020 hadi viwanda 1631 mwaka huu, sawa na ongezeko la viwanda 244 ndani ya miaka minne.

Dkt Samia amefafanua kuwa katika kipindi hicho, viwanda vikubwa vipya 97 vimejengwa, huku vya kati vikiwa 81, ambapo vimetoa ajira za moja kwa moja 21,149 na zisizo za moja kwa moja 60,000. 

“Uwekezaji unaofanyika Pwani na maeneo mengine umeiwezesha nchi yetu kupiga hatua katika mwelekeo wa kujitegemea, kujitegemea kimapato na kibidhaa,”

“Kwa mfano mkoa wa Pwani kuna uzalishaji mkubwa unaofanya tujitegemee katika bidhaa muhimu za ujenzi. Sasa tunajitegemea kwenye bidhaa muhimu za vioo, malumalu, saruji, mabati kule Mkuranga,” amesema Dkt Samia.

Katika hatua nyingine, Dkt Samia amesema miongoni wa ahadi zake kwa Watanzania ni kuchukua hatua za kupunguza gharama za ujenzi ili kutoa fursa kwa wananchi wenye kipato cha chini kujenga nyumba bora za kisasa.

“Mwelekeo wa Serikali ni kuendeleza mpango wa ujenzi wa makazi bora kwa bei nafuu, mkoa wa Pwani umekuwa mfano wa kuibeba ajenda hii,” amesema Dkt Samia.

Leave a Reply