Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kusherehekea Sikukuu za kumaliza mwaka na kuanza mwaka mpya kwa amani na salama.
Pia, amewataka Watanzania wautumie mwaka 2026 kufanya kazi kwa bidii, kuwa na mshikamano, uzalendo na kutimiza malengo waliyojiwekea, ili kuleta uendelevu wa maendeleo.
Amesema Serikali itachukua hatua za kimkakati kuweka mazingira rafiki ya kisera, kisheria na kiutendaji yatakayoongeza fursa za biashara, uwekezaji na fursa nyingine za kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa Watanzania wote.
Sambamba na hayo, amesema Serikali itaendelea kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi bila kusahau wajibu wa kulinda rasilimali za nchi ili zitumike kwa manufaa ya Taifa.
Rais Dkt. Samia ameeleza hayo leo, Jumatano Desemba 31, 2025 katika hotuba yake kwa Taifa aliyoitoa akiwa Ikulu Ndogo ya Tunguu iliyopo Mkoa wa Kusini Unguja visiwani Zanzibar.
