Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake itakamilisha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) mkoani Kigoma, ikipitia Wilaya ya Uvinza.
Amesema reli hiyo ikifika Uvinza, itakwenda hadi Msongati nchini Burundi na Taifa hilo, litaijenga kwenda Afrika Kusini na hivyo kufungua milango ya kufanya biashara.
Dkt Samia ameyasema hayo leo, Jumamosi Septemba 13, 2025 alipozungumza na wananchi wa Uvinja katika mkutano wake wa kampeni za urais.
“Hapa tuna mradi wa ujenzi wa reli ya SGR inayokuja Kigoma. Inatoka Dar es Salaam kuja Kigoma, ikifika Uvinza inakwenda mpaka Msongati kule Burundi, na Burundi wataijenga kwenda Afrika Kusini,” amesema.

Amesema wanafanya hivyo, ili kufungua njia za kufanya biashara, kwa kuwa Bandari ya Dar es Salaam itashusha mizigo na itasafirishwa kwa njia ya reli hadi Jamhuri ya Demokrasi ya Congo (DRC).
Amewataka wakazi wa Uvinja kujiandaa na fursa za kibiashara zitakazotokana na ujenzi wa reli hiyo, akisisitiza ni turufu ya uchumi wa wilaya hiyo.
Sambamba na hilo, ameahidi kukamilisha ujenzi wa barabara mbalimbali za wilaya hiyo kwa kiwango cha lami, ambazo kwa sasa kila unapofika wakati wa mvua hazipitiki.