Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) imeazimia kuanzisha Kituo cha Fedha cha Kimataifa (International Financial Centre) kitakacholenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuongeza upatikanaji wa mitaji, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha fursa za ajira kwa Watanzania.
Akizungumza baada ya kikao cha 38 cha Kikundi Kazi cha TNBC kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya TNBC, Balozi Moses Kusiluka, alisema uamuzi huo umetokana na hitaji la kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Alisema Serikali imekuwa ikisikiliza changamoto zinazowasilishwa na sekta binafsi na kutafuta suluhisho endelevu litakalowezesha wawekezaji kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
“Kutokana na changamoto zilizobainishwa na sekta binafsi, tumefikia makubaliano ya kuanzisha Kituo cha Fedha cha Kimataifa kitakachosaidia kutatua baadhi ya vikwazo vinavyowakabili wawekezaji na kuongeza ushindani wa Tanzania katika kuvutia mitaji ya kimataifa,” alisema Balozi Kusiluka.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha wawekezaji kufanikiwa, kuongeza mapato ya taifa na kutoa ajira kwa Watanzania kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, ambaye aliwasilisha wasilisho la kituo hicho kupitia mapendekezo ya kikundi kazi cha fedha cha TNBC alisema Tanzania imefikia hatua muhimu ya maendeleo ya kiuchumi inayoiwezesha kuanzisha na kuendesha kituo hicho kwa mafanikio.
Alisema tayari nchi sita barani Afrika zina vituo vya aina hiyo zikiwemo Kenya na Rwanda na kutoa ajira za kutosha na kuongeza pato la taifa, na Tanzania itakuwa nchi ya saba kujiunga na orodha hiyo, huku Dar es Salaam ikichaguliwa kuwa eneo bora la kukiweka kutokana na mazingira yake ya kibiashara na miundombinu iliyopo.

“ Uwepo wa Kituo cha Fedha cha Kimataifa utaongeza uwezo wa nchi kuvutia mitaji kutoka ndani na nje ya Afrika, kuwezesha upatikanaji wa fedha za miradi mikubwa ya maendeleo na kuimarisha shughuli za kifedha za kimataifa,” alisema Tutuba.
Alifafanua kuwa kituo hicho kitatoa fursa kwa taasisi za fedha, wawekezaji na kampuni mbalimbali kupata mitaji kwa urahisi zaidi, hatua itakayosaidia kukuza shughuli za kiuchumi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa.
Aidha, alisema kituo hicho kitachochea uhamishaji wa maarifa na teknolojia kwa kuvutia wataalamu wa kimataifa kuja kufanya kazi nchini, jambo litakalosaidia kujenga kizazi chenye ujuzi wa kisasa katika sekta ya fedha na biashara.
“Hii ni fursa muhimu kwa Watanzania kujifunza kutoka kwa wataalamu wa kimataifa na kuimarisha uwezo wao wa kitaaluma katika nyanja mbalimbali za kifedha,” alisema.
Tutuba pia aliwahimiza wafanyabiashara wakubwa na wawekezaji wanaojihusisha na biashara za kimataifa kujiandaa kutumia kituo hicho mara kitakapoanzishwa, akieleza kuwa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) iliyopo itawezesha shughuli nyingi kufanyika kwa urahisi hata kwa wale walioko nje ya nchi.
Alibainisha kuwa Tanzania tayari inakidhi vigezo muhimu vya kuanzishwa kwa kituo hicho kutokana na uwepo wa utulivu wa kisiasa, usalama wa nchi, pamoja na sekta imara ya benki yenye uwezo wa kusimamia shughuli za kifedha kwa viwango vya kimataifa.
Kwa mujibu wa Gavana huyo, wawekezaji watakaotumia kituo hicho watanufaika na fursa ya kufikia soko la zaidi ya watu bilioni 1.4 barani Afrika, kutokana na Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Tunaamini kuwa baada ya Serikali kuridhia rasmi uanzishwaji wa kituo hiki, kutatungwa mfumo wa kisheria utakaochochea uwekezaji na kulinda mitaji ya wawekezaji,” alisema.
Naye Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga, alisema kuanzishwa kwa kituo hicho ni hatua muhimu iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
Alisema kituo hicho kitasaidia kuongeza mtiririko wa mitaji, kuimarisha shughuli za biashara na uwekezaji, pamoja na kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania.
“Mojawapo ya majukumu yetu ni kujenga uwezo wa sekta binafsi na kuweka mazingira yatakayochochea ukuaji wa uchumi kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” alisema Dkt. Wanga.
Mbali na hilo, alisema kikao hicho pia kilikubaliana kuanzisha mfumo wa utoaji wa tuzo kwa taasisi za sekta binafsi na umma ambazo zimeonyesha mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa na utekelezaji wa malengo ya kiuchumi.
Uamuzi wa kuanzishwa kwa Kituo cha Fedha cha Kimataifa umetokana na mapendekezo yaliyotolewa na Kikundi Kazi cha Fedha cha TNBC katika kikao chake cha Machi 2026, ambacho kilibaini umuhimu wa kuwa na mfumo maalumu wa kifedha utakaovutia mitaji zaidi na kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji.
