You are currently viewing Simai: Kuna Yuda serikalini anakwamisha maendeleo
Mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Simai Mohamed Said,

Simai: Kuna Yuda serikalini anakwamisha maendeleo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Simai Mohamed Said, amekemea vitendo vya usaliti vinavyofanywa na baadhi ya viongozi ndani ya Serikali, akisema vinakwenda kinyume na dhamira na juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Simai, ameijenga hoja yake hiyo akiwafananisha viongozi wasaliti na Yuda, huku akiwasihi waache kutumia majina ya viongozi wastaafu na kufanya siasa za 2030 mapema, jambo alilosema linalochonganisha na kuharibu utulivu.

Mbunge huyo, ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma leo, Jumanne Juni 2, 2026 alipochangia hoja katika mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, anaongoza Serikali yake na Watanzania kwa upendo na mshikamano, lakini kufanikiwa kwa Taifa wakati mwingine kuna watu wanaotembea kinyume.

“Leo nambatiza mmoja aliyekuwepo ndani ya Serikali, ni Yuda. Nasema hivyo kwanini, sisi tunataka maendeleo ya nchi yetu, kosa la mama (Dkt Samia) ni wapi? Kwa sababu ya kumuamini mtu kumbe ni Yuda,” amehoji.

Amesisitiza kiongozi huyo msaliti ameibuka hadi katika nyumba za ibada akitafuta huruma za watu na kutumia majina ya viongozi wastaafu ilimradi aonyeshe anapendwa.