You are currently viewing Simba SC. yaitafuna kibabe Gor Mahia

Simba SC. yaitafuna kibabe Gor Mahia

Simba SC imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Tanzania Jumatano usiku.

Mashabiki walijaa uwanjani kushuhudia mtanange huo mkali uliohitimisha Sherehe za Simba Day. Mchezo ulianza kwa kasi ya wastani huku timu zote zikichunguza nguvu za wapinzani.Dakika ya saba, Simba walipata mpira wa adhabu ulioonekana hauna hatari.

Ulinzi wa Gor Mahia ulisahau kumkaba Mohamed Hamza, aliyevunja ukimya kwa kichwa safi kilichomshinda kipa Gad Mathew.

Baada ya mapumziko, Gor Mahia walionekana kuamka lakini walishindwa kutumia nafasi. Dakika za mwanzo za kipindi cha pili, Simba walitumia mpira mrefu kutoka nyuma. Winga wa Simba alijipata na nafasi, akapiga krosi ya chini. Steven Mukwala hakufanya kosa, akiweka mpira wavuni na kuongeza bao la pili.

Ushindi huu umehitimisha maandalizi ya Simba SC kabla ya msimu wa 2025/26. Simba wameimarisha kikosi kwa kusajili wachezaji wapya kama kipa Yakoub Suleiman na mabeki Anthony Mligo, Wilson Nangu, na Rushine De Reuck.

Safu ya kiungo imepata nguvu mpya kupitia Alassane Kante, Semfuko Charles, Morice Abraham, Neo Maema, Naby Camara na Mohammed Bajaber. Washambuliaji Jonathan Sowah na Seleman Mwalimu wameongezwa kusaidiana na Steven Mukwala mbele ya goli. Mashabiki wa Msimbazi wanatarajia moto mpya katika Ligi Kuu Tanzania.

Leave a Reply