Naibu Spika wa Bunge la Seneti la Urusi, Konstantin Kosachev, amepongeza maandalizi ya Tanzania ya Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), akisema nchi hiyo imestahili kuwa mwenyeji wa mkutano huo kutokana na sifa yake katika kudumisha amani, kukuza mazungumzo na kujenga uhusiano wa ushirikiano katika ngazi za kikanda na kimataifa.
Akizungumza katika mahojiano maalum kando ya Mkutano huo unaofanyika jijini Arusha, Kosachev amesema nafasi ya kuandaa Mkutano wa IPU haitolewi kwa kila nchi, bali huzingatia, miongoni mwa mambo mengine, sifa ya nchi, namna inavyoshughulikia masuala ya amani na usalama, pamoja na mahusiano yake na nchi jirani na jumuiya ya kimataifa.
Amesema Tanzania imeendelea kuongeza thamani katika masuala muhimu kwa dunia kupitia mchango wake katika ngazi za ndani, kikanda na kimataifa, hususan katika masuala ya utulivu, usalama na mazungumzo.
“Naamini Tanzania imestahili haki ya kuandaa Mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani, na maandalizi yaliyofanyika hapa yamefanyika kwa kiwango cha juu. IPU ni jukwaa muhimu la kujadili masuala ya amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi,” amesema Kosachev.
