You are currently viewing TANESCO yatangaza siku 6 za maboresho kituo cha umeme Ubungo

TANESCO yatangaza siku 6 za maboresho kituo cha umeme Ubungo

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kuwepo kwa maboresho katika Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Msongo wa Kilovoti 220 cha Ubungo kilichopo jjni Dar es Salaam kuanzia siku ya Jumamosi, tarehe 22 hadi 28 Februari, 2025.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni muhimu kwa Shirika hilo katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja wake kufuatia ongezeko la mahitaji ya matumizi ya umeme katika maeneo ya Zanzibar na Mikoa ya Dar es Salaam, na Pwani.

Ongezeko limesababisha Kituo hicho kuzidiwa na hivyo kulazimu kufungwa kwa Mashineumba (Transformer) mpya kubwa yenye uwezo wa MVA 300 ili kukidhi mahitaji ya umeme katika maeneo tajwa.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Tanesco imesema wakati kazi hizo zitakapofanyika baadhi ya maeneo ya Zanzibar na Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani yataathirika kwa kukosa umeme kwa nyakati tofauti.

Aidha, katika kipindi hicho ambacho huduma ya umeme itakosekana kwa nyakati tofauti Shirika pia litakuwa likifanya matengenezo mbalimbali ya miundombinu ya umeme kwenye maeneo tajwa ili kuiweka miundombinu yetu kwenye hali ya uimara hasa kwenye kipindi hiki tunachoelekea cha msimu wa mvua.

“Shirika linaomba radhi kwa usumbufu katika kipindi chote ambacho huduma ya umeme itakosekana kwenye baadhi ya maeneo na litaendelea kutoa taarifa za maendeleo ya kazi hiyo mpaka kukamilika kwake,” imesema taarifa hiyo.

Leave a Reply