Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika biashara na uwekezaji kwa kuondoa vikwazo visivyo vya lazima, kuboresha huduma mipakani na kuwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika fursa zinazojitokeza.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema hayo leo, Agosti 18, 2026, katika Ikulu Ndogo Zanzibar, baada ya mazungumzo na mgeni wake, Rais wa DRC, Félix Tshisekedi, akieleza kuwa Tanzania na DRC ni nchi marafiki wa muda mrefu ambazo zimekuwa zikifanya biashara kwa miaka mingi, huku takribani asilimia 90 ya mizigo inayoshuka bandarini Tanzania ikielekezwa nchini humo.
Amesema maeneo mengine ya ushirikiano ni ujenzi wa miundombinu jumuishi kwa kuunganisha reli, barabara na usafiri wa majini kupitia Ziwa Tanganyika, hatua itakayosaidia kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuchochea shughuli za kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Rais Samia amesema Tanzania inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) katika mikoa ya magharibi, ambao utasaidia kuvutia uwekezaji na kupanua biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku akiialika DRC kushiriki katika fursa za uwekezaji katika kilimo, uvuvi na mifugo, sekta ambazo Tanzania inaendelea kuimarisha.
Aidha, Rais Samia amempongeza Rais Tshisekedi kwa ujenzi wa barabara ya Makeli-Manono, akisema kukamilika kwake kutaimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na DRC kwa kurahisisha usafirishaji na kuchochea biashara kati ya nchi hizo mbili.
