You are currently viewing Tanzania, Misri kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji

Tanzania, Misri kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji

Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi, amesema Tanzania na Misri zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji kwa lengo la kuleta manufaa kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.

Akizungumza na wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam leo Julai 18, 2026 baada ya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan, El-Sisi amesema mahusiano kati ya Tanzania na Misri yamejengwa katika msingi wa kihistoria wa kuheshimiana na kusaidiana katika nyanja mbalimbali.

Amesema mazungumzo yake na Rais Samia yamekuwa fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili, sambamba na kuendeleza misimamo ya pamoja katika masuala ya kikanda na kimataifa.

Kwa mujibu wa El-Sisi, nchi hizo mbili zimekusudia kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kwa kushirikisha sekta binafsi katika miradi mbalimbali, ikiwamo ujenzi wa miundombinu, nishati, kilimo na viwanda vya dawa na vifaa tiba.

“Nimefurahi sana kukutana na nyinyi leo na natumai kuendelea kuwepo ushirikiano kwa maslahi ya nchi zetu mbili na Afrika kwa ujumla. Natamani nchi hii ya Tanzania ipate kheri na utulivu,” amesema.