Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesema ifikapo Julai mwaka huu, huenda meli ya kwanza ikasafiri kutoka Tanga nchini Tanzania kusafirisha mafuta yanayotokana na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwenda kuuza mataifa ya nje.
Hatua hiyo ni baada ya matarajio ya kukamilika kwa mradi huo, ambao mkataba wa mwisho wa uwekezaji kati ya nchi hizo, ulisainiwa Februari 1, mwaka 2022, kuruhusu utekelezaji na hatimaye uko mbioni kukamilika.
Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi Februari 7, 2026 mbele ya waandishi wa habari, baada ya kikao cha uwili na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, aliyepo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
“Tunamshukuru Mungu na tunashukuru ndugu zetu kwa mazungumzo yetu, kuanzia Julai, huenda meli ya kwanza ikaondoka pale Tanga kwenda mafuta yanakopelekwa,” amesema.
Kwa upande wake Rais Museveni, amesema baada ya uhuru mataifa hayo yanapaswa kusonga mbele badala ya kurudi nyuma, hasa ukizingatia tayari kumeshaanza kuonekana viashiria vya hatari.
“Nchi kubwa zinaweza kutuwekea mashinikizo, lakini namna unavyoyazuia inategemea na nguvu ulizonazo. Tumeona India ilivyotishwa na mataifa kadhaa, lakini ilikuwa na nguvu ya kusema hapana na India ni India sasa na imeweza kukua,” amesema.
