You are currently viewing Tanzania, Uganda zakubaliana kuondoa vikwazo kuharakisha biashara

Tanzania, Uganda zakubaliana kuondoa vikwazo kuharakisha biashara

Tanzania na Uganda zimekubaliana kuharakisha utatuzi wa vikwazo vya biashara, kupanua masoko ya bidhaa zao na kuboresha usafirishaji ili kukuza biashara na uwekezaji kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Hayo yamefikiwa leo tarehe 18 Novemba, 2026, wakati Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipoanza Ziara ya Kitaifa ya siku mbili nchini Uganda. 

Mapema leo asubuhi, Rais Samia aliwasili Ikulu ya Entebbe na kupokelewa na mnwenyeji wake, Yoweri Kaguta Museveni, Rais ya Uganda.

Katika mazungumzo rasmi baina yao, wamejadili namna ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa nchi zao, kuongeza biashara na uwekezaji, kurahisisha upatikanaji wa masoko na kuondoa vikwazo vinavyoathiri usafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na Uganda.

Rais Dkt. Samia amesema Tanzania na Uganda zimepiga hatua katika kutekeleza maamuzi ya awali kuhusu biashara, uwekezaji, nishati, usafiri na miundombinu.

Ametaja changamoto za usafiri na usafirishaji kuwa miongoni mwa sababu zinazorudisha nyuma ukuaji wa biashara, na kueleza hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kuboresha miundombinu hiyo.

Rais Dkt. Samia amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Uganda katika mradi wa reli ya kisasa utakaounganisha Isaka na maeneo ya mpakani na Uganda.

Tanzania itaendelea kushirikiana na Uganda kwa moyo wa watu wamoja, hatima moja. Sasa ni wakati wa kuharakisha utekelezaji wa tuliyokubaliana,” amesema Rais Dkt. Samia, akibainisha hatua za upanuzi na maboresho ya Bandari za Dar es Salaam na Tanga kuwa sehemu ya jitihada za kuboresha usafiri na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Pia, Rais Dkt. Samia ameipongeza Uganda kwa kuanza ujenzi wa ubalozi wake katika Miji

wa Serikali Dodoma, ikiwa ni Taifa la kwanza kufanya hivyo tangu kuzinduliwa kwa Mji huo.

Kwa upande wake, Rais Museveni amesema biashara kati ya Tanzania na Uganda inapaswa kuzingatia mahitaji ya pamoja, akitolea mfano wa mchele wa Tanzania wenye uhitaji mkubwa nchini Uganda, na sukari inayozalishwa Uganda yenye soko kubwa nchini Tanzania.

Ameongeza kuwa, Uganda ina ziada kubwa ya sukari, huku wananchi wake wakinunua mchele wa Tanzania kwa kuwa ni bora na wa bei nafuu.

Rais Museveni pia ameonya dhidi ya hatari ya shinikizo la ndani la kuzuia bidhaa zinazotoka nchi moja kwenda nyingine, na namna linavyoweza kudhoofisha uzalishaji, na kushusha uhusiano wa kibiashara baina ya Tanzania na Uganda.

“Tunahitaji maliasili, uzalishaji wa bidhaa, soko la kutosha na mawasiliano,” amesema Rais Museveni, akisisitiza kuwa nchi za Afrika zinahitaji kuunganisha nguvu katika usimamizi wa rasilimali kwa manufaa ya wananchi wao.

Viongozi hao pia wamejadili ushirikiano katika sekta ya nishati, ikiwemo usafishaji wa mafuta na uratibu wa miradi ya viwanda katika nchỉ hizo, ambapo Rais Museveni amesema nchi yake inapanga kujenga kiwanda kidogo cha kusafisha mafuta Hoima na inaunga mkono ujenzi wa kiwanda kikubwa zaidi jijini Tanga, Tanzania.

Kwa pamoja, wamehimiza utekelezaji wa haraka wa makubaliano yaliyofikiwa.