You are currently viewing TAWA yajipanga kununua ndege nyuki 4 kukabili tembo

TAWA yajipanga kununua ndege nyuki 4 kukabili tembo

Na Mwandishi Wetu, Ruvuma

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA inatarajia kununua ndege nyuki nne aina ya DJI Mavic 3 ambazo zitapelekwa katika wilaya za Namtumbo mkoani Ruvuma na Liwale, Nachingwea na Lindi mkoani Lindi ili kukabiliana na wanyamapori wakali waharibifu hususani tembo.

Hayo yamebainishwa jana tarehe 15 Oktoba, 2024 na Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, Mabula Nyanda mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati wa ziara ya kufuatilia utakelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa mkoani humo  Septemba 28, 2024  kuhusu udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu katika wilaya za Namtumbo na Tunduru.

Pia Mabula amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 TAWA inatarajia kuajiri Askari 351 ambao watapangiwa vituo vilivyopo kwenye maeneo yenye changamoto kubwa ya wanyamapori hao.

Amesema askari 20 watapangiwa katika kituo kidogo cha Songea na watafanya kazi katika wilaya za Tunduru na Namtumbo, wilaya zinazotajwa kuwa na changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Aidha, amesisitiza kuwa TAWA inatarajia kununua gari moja na pikipiki mbili ambavyo vitapelekwa kituo kidogo cha Songea na vitatumika Katika kudhibiti changamoto ya wanyamapori hao katika wilaya za Tunduru na Namtumbo.

Pia, Mamlaka itaboresha kituo kimoja cha Askari cha kudumu katika wilaya ya Tunduru na vikosi viwili vya kudumu vya Askari kutokea kituo kidogo cha Songea ili kurahisisha mwitikio wa haraka wa matukio ya tembo.

Kamishna Mabula ameongeza kusema kuwa baada ya changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kuendelea kuonekana inakuwa kubwa, Wizara ya Maliasili na Utalii iliandaa Mkakati wa kukabiliana na migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu ambao unatekelezwa na Taasisi za Wizara zilizo chini ya Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu (TAWA , TANAPA, NCAA na TFS) kwa kugawana maeneo, Halmashauri za Wilaya, Taasisi zisizo za kiserikali, wadau wa Uhifadhi na wananchi kwa ujumla

Aidha, katika hatua nyingine kutokana na uwepo wa bustani ya wanyamapori hai inayosimamiwa na TAWA (Ruhila Zoo) katika Manispaa ya Songea, bustani inayotajwa kuwa ni kivutio kikubwa kwa wakazi wa Mkoa huo, Kamishna Mabula amemuomba Mkuu huyo wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed kusaidia ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Kilometa 5 ambayo itafika moja kwa moja katika bustani hiyo ili kuwawezesha wakazi wa Mkoa huo kufika kirahisi katika kivutio hicho cha utalii.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amempongeza Kamishna huyo kwa hatua za haraka alizochukua za kufuatilia utakelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kufuatia maelekezo aliyoyatoa alipokuwa katika ziara yake mkoani humo mwezi Septemba, 2024.

Kanali Ahmed Abbas Ahmed pia ameipongeza TAWA kwa jitihada walizochukua kama mipango ya muda mfupi na muda mrefu katika kukabiliana na changamoto hiyo mkoani humo na kukiri kuwa jitihada hizo zinarudisha matumaini kwa wananchi wa Ruvuma kwa kuwa zinalenga kuimarisha usalama wa maisha na mali zao dhidi ya uvamizi wa wanyamapori kwenye maeneo ya wananchi hao.

Leave a Reply