You are currently viewing TEMEKE, EVER GREEN wapanda miti 500 maadhimisho wiki ya mazingira duniani
Screenshot

TEMEKE, EVER GREEN wapanda miti 500 maadhimisho wiki ya mazingira duniani

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WILAYA ya Temeke kwa kushirikiana na Kampuni ya Ever Green Landscaping Co. Ltd imepanda miti zaidi ya 500 katika maadhimisho ya Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 kwa lengo la kuhamasisha na kuendeleza uhifadhi wa mazingira.

Pia katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuweka jiji hilo safi, mbali na upandaji miti kando ya Barabara ya Mandela katika Kata ya Kurasini, jijini Dar es Salaam pia kampuni hiyo iliungana na wilaya hiyo kushiriki usafi wa mazingira katika eneo hilo.

Screenshot

Miti hiyo ilipandwa katika eneo lenye urefu wa kilomita tatu kuanzia Uhasibu hadi makutano ya Oilcom, huku shughuli za usafi zikifanyika katika eneo lote kwa ushirikiano wa wananchi, viongozi wa serikali, taasisi mbalimbali na wadau wa sekta binafsi.

Akizindua kampeni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, aliwataka wakazi wote wa wilaya hiyo kushiriki kikamilifu katika juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yao ya makazi.

“Iwe wewe ni mpangaji au mwenye nyumba, kama unaishi Temeke lazima uwe na miti mitano. Chagua mwenyewe kama ni miti ya matunda au ya kivuli,” alisema Mapunda.

Alisema upandaji miti ni moja ya njia rahisi na za gharama nafuu zinazoweza kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na changamoto zinazotokana na ongezeko la idadi ya watu katika maeneo ya mijini.

Akizungumzia mpango huo wa upandaji miti, Mkurugenzi mtendaji wa kampu Kampuni ya Ever Green Landscaping, Amir Mpungwe alisema mpango huo unatokana programu ya Green Corridor Initiative— programu ya muda mrefu ya ngazi ya jiji inayolenga kuanzisha na kuunganisha njia za kijani katika barabara kuu, maeneo ya umma na makazi mbalimbali jijini Dar es Salaam.

“Dhana ya mpango huu ni rahisi lakini yenye athari chanya kwa jamii. Badala ya kupanda miti katika makundi madogo yaliyotawanyika ambayo yana mchango mdogo kwa mazingira, Green Corridor Initiative inalenga kuunda mistari endelevu ya miti inayotoa kivuli katika maeneo muhimu ya mijini. 

“Haya ni maeneo ya barabara na sehemu za umma ambapo miti inaweza kupandwa kwa utaratibu maalumu, kutunzwa kitaalamu na kuachwa ikue ili kuwa miundombinu hai inayotoa kivuli, kusafisha hewa na kupunguza joto, kwa manufaa ya wakazi wote wa jiji,” alisema 

Alisema ukanda wa Barabara ya Mandela uliopo Kurasini, Temeke — ambapo Ever Green imepanda zaidi ya miti 500 — ni mfano wa kwanza mkubwa unaoonesha utekelezaji wa mpango huu kwa vitendo. 

“Hata hivyo, huu si mwisho wa safari hiyo. Dira ya mpango huu ni kuona njia hizi za kijani zikienea katika manispaa zote tatu za Dar es Salaam — Temeke, Ilala na Kinondoni — na hivyo kubadilisha sura ya jiji hatua kwa hatua, mtaa kwa mtaa na eneo kwa eneo.

“Tunawashukuru pia wadau wetu  

Bytrade, NatureRipe Kilimanjaro

Limited na Mabwepande Compost Facility kwa kutuunga mkono kwa sababu jukumu la kutunza mazingira si la serikali pekee bali linahitaji ushiriki wa kila mwananchi ili kuhakikisha maeneo ya makazi yanakuwa safi.

Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni na ilianzishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1972 kufuatia Mkutano wa Kimataifa wa Mazingira ya Binadamu uliofanyika Stockholm, Sweden.