You are currently viewing TPSF yasifu viongozi wa BoT na TRA kwa utendaji uliotukuka

TPSF yasifu viongozi wa BoT na TRA kwa utendaji uliotukuka

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) imesema  inatambua na kuthamini uongozi na utendaji  kazi wa viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kwamba ina kila sababu ya kuwapa tuzo viongozi hao kwa utendaji kazi wao.

Akieleza kauli hiyo  katika kikao cha 38 cha Kamati Tendaji ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Mwenyekiti wa TPSF, Bi Angelina Ngalula, alisema  kuwa Gavana wa BoT, Bw Emmanuel Tutuba, na Kamishina Mkuu wa TRA, Bw Yusuph Mwenda,  ni nguzo muhimu ya utendaji wa kazi katika taasisi zao.

 “Sisi katika sekta binafsi tunafurahishwa sana na utendaji kazi wa viongozi hawa katika kusimamia weledi na ufanisi katika taasisi wanazoziongoza”, alisema Bi Ngalula na kuongeza kuwa sekta binafsi ina kila sababu ya kuwapa tuzo kwa utendajikazi wao.

Mwenyekiti huyo alisema siyo kosa kwa sekta binafsi kutambua umuhimu na utendajikazi wa viongozi hao katika kusimamia majukumu ya watendaji walio chini yao.

Gavana wa Benki ya Tanzania (BoT) Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) akiteta jambo na Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw.Yusuph Mwenda mala baada ya kumalizika kwa kikao cha 38 cha Kamati ya Utendaji ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), kilichojadili masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Kauli ya Bi Ngalula iliungwa mkono na Katibu Mkuu Kiongozi na Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya TNBC, Balozi Moses Kusiluka. Balozi Dkt Kusiluka  alisema kuwa utendaji kazi katika serikali umebadilika na kuimarika sana kutokana na mageuzi makubwa ambayo yamefanyika.

“Ni ukweli usiopingika kuwa watendaji wengi katika sekta ya umma wamebadilika na wanafanyakazi vizuri na kazi hiyo inaonekana”, alisema Dkt Kusiluka na kueleza kwamba mabadiliko ni suala la muda kwa kuwa binadamu wanabadilika siku hadi siku. Alisema hivyo ushuhuda unaotolewa na sekta binafsi unaonesha ni namna gani serikali ilivyodhamiria  kuwahudumia wananchi.

“Tutaendelea kuhimizana na kuhakikisha kila mtendaji wa taasisi anawajibika na kuleta matokeo chanya kwa taasisi anayoihudumia,”alisema Dkt Kusiluka.

Alisema kwamba viongozi hao wawili taasisi wanazoziongoza ni ngumu na kazi  zao ni ngumu pia maana kazi zao zinaendana na malengo; pongezi zinazotolewa kwao wanazistahili, alisema.

“Hawa viongozi wanafanyakazi ngumu kweli kweli na hivyo matokeo  yanayopatikana yametokana na usimamizi wao bora, hivyo wanastahili pongezi,” alisema Dkt Kusiluka na kuwataka watendaji wengine kuiga ari ya ufanyajikazi waliyonayo viongozi hao wawili.

Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt Godwill Wanga, naye aliunga mkono pongezi zilizotolewa kwa viongozi hao, na kudokeza kuwa TNBC ina mpango wa kutoa tuzo kwa taasisi za umma na binafsi ambazo zitakua zikitoa mchango chanya kwa serikali na wadau wengine wa maendeleo.