You are currently viewing TRA yakusanya trilioni 3.58 mwezi Machi 2026
Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda

TRA yakusanya trilioni 3.58 mwezi Machi 2026

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 3.58 kwa mwezi Machi pekee sawa na ufanisi wa asilimia 107.6 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 3.32 makusanyo ambayo yamechangiwa na ukaribu uliopo baina ya Mamlaka hiyo na walipakodi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda April 1, 2026 imeeleza kuwa Makusanyo hayo ya mwezi Machi yanapelekea TRA kuwa imekusanya kiasi cha kiasi cha shilingi trilioni 9.31 sawa na ufanisi wa asilimia 106.4 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 8.75, katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26 (Januari hadi Machi 2026).

Makusanyo hayo ya kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/26, ni sawa na ukuaji wa asilimia 23.6 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi trilioni 7.53 kilichokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/25.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Ufanisi wa makusanyo kwa mwezi Machi unapelekea TRA kuweza kuandika rekodi mpya za kipekee katika ukusanyaji wa mapato nchini Wastani wa Makusanyo kwa mwezi katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025/26 umefikia shilingi trilioni 3.10 ambacho ni kiasi cha juu kabisa ukilinganisha na wastani wa shilingi trilioni 2.51  kwa kipindi kama hicho mwaka 2024/25.

TRA imeweza kurekodi Ukuaji chanya wa asilimia 23.6 katika kipindi cha Januari -Machi 2026, na imeweza kulifikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi 21 mfululizo kuanzia mwezi Julai 2024, mafanikio ambayo Mamlaka haijawahi yafikia toka ianzishwe.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kwa kipindi hicho chote, Mamlaka imeweza kuwa na Wastani wa ufanisi wa utendaji wa shilingi trilioni 2.87 kwa kila mwezi.

Ufanisi huu wa makusanyo katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2025/26 ni muendelezo kwa vitendo wa utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuhakikisha kuwa Mamlaka inaongeza makusanyo ya kodi kwa kuongeza hali ya ulipaji kodi kwa hiari nchini.

Imeeleza kuwa Makusanyo yaliyokusanywa kwenye robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2025/26 ni sawa na ukuaji wa asilimia 114.1.