Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Shirika la Reli Tanzania (TRC), limetangaza kuanza kwa safari ya treni ya haraka (express train) ya reli ya kiwango cha kimataifa – SGR ambayo itakuwa ikifanya safari kati ya Dar es Salaam na Morogoro bila kusimama vituo vya kati.
Taarifa iliyotolewa leo Julai Mosi,2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano -TRC, Jamila Mbarouk imesema ujio wa treni hiyo umekuja na mabadiliko ya ratiba za treni kati ya Dar es Salaam na Morogoro kuanzia Julai 5, 2024.
Amesema treni ya haraka itakuwa ikiondoka Dar es Salaam saa 12:00 asubuhi na saa 1:10 usiku, na itaondoka Morogoro saa 12:20 asubuhi na saa 1:30 usiku.
Treni ya kawaida itakuwa ikiondoka Dar es Salaam saa 3:30 asubuhi na saa 10:00 jioni na itaondoka Morogoro saa 3:50 asubuhi na saa 10:20 jioni.
Amewashauri abiria kukata tiketi kupitia njia ya mtandao au madirisha ya tiketi yaliyo ndani ya vituo vya treni saa mbili kabla ya muda wa safari ili kuepuka msongamano.
Amesema shirika litaendelea kuongeza idadi ya safari kulingana na ongezeko la idadi ya abiria ili kutoa huduma bora na za uhakika.