Rais Donald Trump wa Marekani amempa Rais Vladimir Putin wa Urusi siku 10-12 za kusimamisha mauaji nchini Ukraine, zikiwa ni pungufu kutoka siku 50 alizozitoa kwa kiongozi huyo wa Urusi wiki mbili zilizopita.
“Hakuna sababu ya kungoja,” Trump alisema alipotoa muda huo mwingine ambao ni mfupi zaidi tofauti na siku 50 alizozitoa awali. “Hatuoni hatua yoyote ikipigwa. “Ni lazima Putin afanye makubaliano. Watu wengi sana wanakufa,” Trump alisema wakati wa ziara yake ya Scotland.
Trump alirudia tena kumkosoa Putin kwa kuzungumza juu ya kuvimaliza vita huku akiendelea kuwashambulia raia wa Ukraine. “Na ninasema, hiyo sio namna ya kusonga mbele,” Trump alisema na kuongeza, “mimi nakatishwa tamaa na Rais Putin.”
Alipoulizwa kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na uwezekano wa mkutano na Rais Putin, Trump alisema “sina mpango wa kuzungumza zaidi.”