Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko la Machinga Complex jijini Dodoma, Marico Magale, amesema wamachinga wa soko hilo wamepokea na kuunga mkono kauli ya Serikali ya kusitishwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, wakieleza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda amani na usalama wa nchi.
Magale amesema wamachinga wanaelewa madhumuni ya maelekezo hayo yaliyotolewa bungeni leo, Juni 26, 2026, akisisitiza kuwa baadhi ya kauli za kisiasa zinaweza kuchochea hisia na kuongeza taharuki miongoni mwa wananchi.
Akirejea matukio ya Oktoba 29 yaliyowahi kuathiri shughuli zao za biashara, amesema wafanyabiashara wa Machinga Complex walikuwa miongoni mwa waathirika wakubwa, hali iliyowapa uzoefu wa athari zinazoweza kusababishwa na maandamano.
“Maisha yetu sisi wamachinga yanategemea biashara za kila siku. Hatuwezi kupata kipato bila kutoka kufanya biashara. Kwa hiyo tunafahamu kuwa maandamano hayawezi kufanyika huku biashara zikiendelea kama kawaida,” amesema.
