You are currently viewing ‘Ushirikiano wa kisiasa wa Tanzania, Singapore ugeuzwe kuwa fursa za biashara’

‘Ushirikiano wa kisiasa wa Tanzania, Singapore ugeuzwe kuwa fursa za biashara’

Shirikisho la Biashara la Singapore (SBF) limezitaka sekta binafsi za Tanzania na Singapore kutumia ushirikiano wa kisiasa uliopo kuibua fursa za biashara na uwekezaji katika Soko la Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa SBF, Mark Lee, alipozungumza katika Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Singapore.

Amesema lengo la ushirikiano huo ni kugeuza mahusiano mazuri ya kisiasa kuwa matokeo ya kibiashara yenye manufaa kwa pande zote.

Tangu mwaka 1997, amesema Singapore imetekeleza miradi 36 ya uwekezaji nchini Tanzania yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 500 na kuzalisha ajira zaidi ya 3,000, huku akibainisha kuwa bado kuna fursa kubwa za kupanua ushirikiano huo.

Lee amesema ujio wa ujumbe wa kampuni 15 kutoka Singapore ni hatua ya mwanzo kuelekea ushirikiano zaidi katika sekta za miundombinu ya viwanda, usafirishaji na ugavi, biashara ya bidhaa, kilimo, teknolojia na huduma za teknolojia kwa biashara.

“Hatukuja kuvuna faida pekee, bali kushirikiana kwa pamoja kujenga uchumi wa pande zote,” amesema.