MATUNDA ya Uwekezaji wa Sh. 429 bilioni uliofanywa na Serikali katika Bandari ya Tanga umeanza kulipa kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya meli zinazopitisha shehena kutoka meli 197 kwa mwaka 2022/2023 hadi kufikia meli 307 kwa mwaka 2023/2024.
Hayo yamebainishwa jana Jumanne na Meneja wa Bandari ya Tanga, Mrisha Masoud akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuipokea meli ya XINHAITONG 50 iliyotoka nchini China moja kwa moja kuleta shehena ya magari kupitia kampuni ya Meli ya SeaFront Shipping Services Limited (SSS).
Alisema ujio wa meli hizo na kushusha magari katika bandari hiyo inadhihirisha kwamba ufanisi mkubwa katika shughuli za kupakia na kupakua zimaimarika kutokana na maboresho hayo makubwa.
“Lakini niseme kwamba maboresho haya pia yameleta ongezeko kubwa la ajira na hadi sasa idadi ya makampuni ya wakala wa usafirishaji katika bandari yameongezeka kutoka 32 hadi 132,” alisema.
Akizungumzia kuhusu ongezeko la mapato katika bandari hiyo alisema kwamba yameongezeka kutoka Sh 16 bilioni mwaka wa fedha 2022/2023 hadi kufikia Sh 18.6 bilioni kwa mwaka 2023/2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 74.1.
“Ongezeko hilo la mapato linatokana na maboresho yaliyofanyika katika bandari ya Tanga na ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi kwa ujumla,“ alisema.
Alisema kwamba maboresho haya yanaonyesha jinsi uwekezaji katika miundombinu unavyoweza kuleta matokeo chanya kwa jamii na uchumi wa Taifa.
Hata hivyo, alisema Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha sekta ya usafirishaji ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kitovu cha biashara katika eneo la Afrika Mashariki.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Afisa Uhusiano wa TPA nchini Enock Bwigane amesema wanamshukuru mdau wa kampuni ya Sea Front ambaye amefanikisha kuwasili kwa meli hiyo iliyobeba shehena mchanganyiko yakiwemo magari zaidi ya 350.
Bwigane alisema kwamba asilimia kubwa ya shehena hiyo inaelekea nje ya nchi na kuwepo kwa meli hiyo ambayo inahudumiwa kwa saa 48 tangu ifike leo jana alfariji inafikisha meli idadi ya meli 12 ambazo zimehudumiwa na mteja wao Kampuni ya Sea Front Shipping.
Alisema kwamba mteja wao huyo alikuwa akifanya huduma za kibandari katika Bandari ya Dar es salaam lakini kutokana ana uwekezaji uliofanywa na Serikali wa 429.1 bilioni kwa awamu zote mbili kuboresha bandari ya Tanga umesababisha meli kubwa nyingi kwa shehena tofauti kuhudumiwa katika Bandari ya Tanga.
“Huyu ni mteja mojawapo alileta meli kutoka nchini China na ambapo meli hii imefikisha idadi ya meli 12 ambazo zimeshuhudumiwa na tunapoongelea ufanisi wa mapato katika Bandari ya Tanga tunajivunia,” alisema.
Alisema robo ya kwanza ya Julai Mosi hadi Septemba 30 mwaka huu bandari hiyo ilikusanya bilioni 18.6 na bilioni 8 katika mapato hayo zimetokana na mteja huyo ambaye amekwisha kuwezesha ujio wa meli 12 katika Bandari hiyo.
“Tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu kwa maamuzi yake ya kufanya maboresho katika Bandari zote nchini ikiwemo Bandari ya Tanga ambapouwekezaji mkubwa uliofanyika umesaidia kuongeza ufanisi katika Bandari na mapato yameongezeka na huduma ya shehena zimeongezeka kila mwaka ukiangalia kwa miaka miwili iliyopita,” alisema.
Alisema huduma katika bandari hiyo zimeongezeka kutoka kuhudumia shehena tani 800,000 hadi tani milioni 1.5 na mwaka huu wanatarajia kuhudumia shehena tani milioni 1.4 katika robo ya kwanza na wameshahudumia shehena tani 300,000.
Aidha, alisema katika Bandari ya Tanga wanahudumia shehena kwa ushoroba wa Kanda ya Kaskazini na wanafarajika kwa mara ya kwanza kwa nchi ya DRC na Zambia mzigo mkubwa unaopita hapo ni Copper ambapo zaidi ya tani 30,000.
Alisema katika meli hiyo iliyokuja kuna mizigo mchanganyiko unakwenda Rwanda katika mchanganyiko wao na wao kama Bandari wanafarijika kwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika Bandari.
“Tunasema kwamba baada ya uwekezaji katika Bandari ya Tanga umelipa ni jambo ambalo tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu na tumefarijika nasi tunamuhaidi kwamba hatutamuangusha tutafanya kazi kwa bidii na kuongeza mapato ili kuimarisha uchumi wa nchi,” alisema Bwigane.